Na Baraka Mbolembole
Ni mechi nyingine ngumu kwa kikosi hicho kilichoshinda
mataji 25 katika ligi ya Bara. Ikiwa na kumbukumbu ya kufika hatua ya makundi
mara moja mwaka 1998, hakika miaka karibia 20 sasa Yanga wanakidhi viwango vya
kuvunja rekodi yao hiyo na kufuzu kwa mara ya pili makundi ya ligi ya mabingwa
Afrika-michuano mikubwa zaidi ya vilabu barani Afrika.
ILIPOTOKA MIAKA 18 ILIYOPITA…..
Yanga ‘ilibatizwa’ jina la ‘Jamvi la Wageni’ baada ya
kupokea vipigo vya 6-0, 4-0 ilipofuzu
kwa mara ya kwanza hatua ya makundi katika ligi ya mabingwa mwaka 1998. Vipigo
hivyo vilitoka kwa Raja Casablanca ya Morocco
na Maning Rangers ya Afrika
Kusini na walimaliza mechi sita za makundi wakiwa na alama mbili tu, baada ya
kuambulia sare Dar es Salaam dhidi ya Raja na Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Tangu wakati huo imefanikiwa kushinda mataji tyisa ya ligi
kuu Tanzania Bara ( 2002, 2005, 2006, 2007/08, 2008/09, 2010/11, 2012/13,
2014/15, 2015/16,) imeshinda mataji mawili ya klabu bingwa Afrika Mashariki na
Kati ( 2011 na 2012,) pia wameshinda mataji ya Ngao ya Jamii na FA Cup ndani ya
Tanzania bara.
Hii inamaanisha wameendelea kujiimarisha katika soka la
ndani, hivyo wanapaswa kutumia uzoefu na mafanikio yao hayo kuifunga Zanaco
timu ambayo imeshinda ubingwa wa ligi kuu Zambia mara Saba tu huku wakifanya
hivyo ndani ya miaka hii 15 (2002, 2003, 2005, 2006, 2009, 2012, 2016)
Mafanikio makubwa ya timu hiyo ya Zambia katika ligi ya
mabingwa ni kufika hatua ya 16 bora na walifanya hivyo mwaka 2010 walipocheza
kwa mara ya tano ya mwisho.
Mwaka 2003 walicheza kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya
mabingwa na kuishia raundi ya kwanza, wakarejea tena mwaka 2004 safari hii
waliishia raundi ya pili baada ya kuwaondoa Simba SC ya Tanzania bara katika
raundi ya kwanza kwa jumla ya magoli 2-1.
Kwa
kutumia uzoefu wa kushiriki mara ya 22 sasa michuano ya mabingwa Afrika,naamini
Yanga hawapaswi kuidharau hata kidogo Zanaco lakini ni lazima waitumie kama
‘ngazi’ ya kupandia kwenye kilele cha mafanikio. Yanga wana uzoefu wa kutosha
sasa wa kuwaondoa timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1985
Yanga
wanacheza michuano yao ya tisa ya klabu bingwa tangu walipofuzu kwa mara ya
mwisho hatua ya makundi,na mara tatu wamefanikiwa kufika hatua ya mwisho kabla
ya kufuzu kwa hatua ya makundi. Walifanya hivyo miaka ya 2001, 2007 na 2016.
NI WAKATI
WA WACHEZAJI WA KIGENI ‘KUULIPA’ MPIRA WA TANZANIA
Mlinzi wa
kati raia wa Togo, Vicent Bossou, viungo Mzimbabwe, Thaban Kamusoko, Mnyarwanda,Haruna
Niyonzima, Mzambia,Justine Zulu na washambuliaji,Mzambia,Obrey Chirwa,
Mrundi,Amis Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma wameshafanya kazi nzuri ndani ya
kikosi cha Yanga.
Ukiachana
na Wazambia, Zulu na Chirwa, wachezaji hao wengine wa kigeni walikuwepo katika
kikosi cha timu hiyo kilichoshinda mataji ya FA Cup na ligi kuumsimu
uliopita,na walikuwa sehemu ya timu iliyotolewa hatua ya 16 bora katika ligi
mabingwa Afrika na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya magoli 3-2 na kungukia katika
Confederation Cup ambako walifanikiwa kufika hatua ya makundi kwa mara ya
kwanza.
Hakika
wachezaji hao wa kigeni walikuwa na mchango mkubwa sana katika msimu wao wa
kwanza klabuni Yanga,na hilo ndiyo lilichochea Chirwa kusajiliwa kwa thamani
isiyopungua milioni 200 kutoka Platnum FC ya Zimbabwe naa kuweka rekodi ya
mchezaji ghali zaidi katika soka la Tanzania.
Kama klabu
inatumia hadi milioni 200 kumsaini mchezaji wa kigeni na kumlipa mshahara
usiopungua milioni 8 kwa mwezi bila shaka inataraji makubwa zaidi kutoka kwa
mchezaji husika na kwa Yanga sasa wana kiu kubwa ya kuhakikisha wafuzu kwa
hatua ya makundi katika michuano ya ligi ya mabingwa.
Ili jambo
hilo liwezekane kila mchezaji anapaswa kujituma,kuwa na nia na utayari wa
kupambana kuhakikisha hilo linatokea.
Ukitazama
katika kikosi cha Yanga kuelekea mchezo wa Jumamosi hii dhidi ya Zesco
utagundua kuwa kocha Mzambia,George Lwandamina na wasaidizi wake Juma Mwambusi
na Juma Pondamali wanakabiliwa na changamoto ya kutengeneza timu mpya kutoka
katika kikosi kile kilichokuwa chini ya kocha aliyepita Mholland,Hans van der
Pluijm.
Na
mabadiliko hayo yanapaswa kufanyika si kwa kupenda bali kutokana na maumivu
ambayo yamekuwa kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kama beki namba
mbili,Juma Abdul, Niyonzima,Kamusoko, Ngoma na Tambwe. Hawa ni wachezaji watano
ambao wameifikisha Yanga hapo ilipo,na sasa jambo la kujiuliza je, wachezaji wengine wanaweza kupigana na kuziba mapengo
ya wachezaji hao?
Hassan
Kessy nimzuri sana katika ushambuliaji, lakini tatizo lake kubwa ni kupenda
kuuchezea sana mpira na kukimbia nao. Tofauti na Juma Abdul ambaye yeye
hushambulia sana kwa kutegemea uwezo wake wa kupiga krosi za mbali na pasi
zinazofika.
Mechi za
kimataifa ni ngeni kwa Kessy na endapo atapewa nafasi ningependa acheze kwa
umakini kama anavyofanya Juma na asipendeleee sana kukimbia na mpira hadi
katika lango la wapinzani kwa sababu jambo linaweza kutoa ‘mwanya’ kwa Zanaco
na kutumia mipira ya ‘kustukiza’ kupitia upande wake.
Ni ngumu
sana kuziba mapengo ya Thaban na Niyonzima kwa aina ya wachezaji waliopo sasa
katika timu ya Yanga, lakini ikitokea wawili hao kukosekana hakuna namna
itawabidi benchi la ufundi kuwaandaa Said Juma Makapu, na Juma Mahadhi ambaye
alipata majeraha pia katika mchezo wa FA Cup siku ya Jumanne hii dhidi ya
Kiluvya United.
Licha ya
kufunga magoli 14 hadi sasa katika michuano yote, Chirwa ni mchezaji ambaye
anahitaji msaada wa Ngoma au Tambwe ili kuendelea kufunga magoli. Uwezo wa
chini kutoka kwa Malimi Busungu katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar
wikendi iliyopita ni kielelezo tosha kuwa mchezaji huyo si wa kumtegemea
kuibeba timu katika mchezo dhidi ya Zanaco.
EmmanuelMartin
bado anaendelea kujipambanua hivyo kuwakosa Tambwe na Ngoma ni ‘jambo baya’ kwa
Yanga kuelekea mchezo wa Jumamosi hii ambao ni muhimu kushinda. Kama wachezaji
hao wa kigeni watakuwepo basi huu ni wakati wao wa kuilipa Yanga na kuifikisha
hatua ya makundi katika ligi ya mabingwa Afrika.
TATIZO LA
SAFU YA ULINZI….
Udhaifu
mkubwa wa kikosi cha Yanga lipo katika eneo la ulinzi,japokuwa wanaonekana kuwa
na wachezaji wazuri,lakimni ukweli maelewano ya walinzi wa kati si mazuri, na
hilo ndilo lilichangia ‘maumivu’ ya kufungwa 4-0 na Azam FC katika michuano ya
Mapinduzi Cup hata katika michezo dhidi ya Mbeya City FC, Simba SC na Tanzania
Prisons tatizo hilo liliwangusha.
Unapokuwa
na kipa bora kama Deogratius Munish ‘Dida’ unatakiwa kufanya makosa makubwa
katika beki ili kuruhusu nyavu zako kufikiwa na mpira mara kwa mara na hilo
ndilo limekuwa likifanya na walinzi wa kati wa Yanga. Iwe,Bossou na Kelvin
Yondan, Nadir na Bossou,Nadir na Kelvin,Vicent Andrew na Bossou,Andrew na
Kelvin au Nadir na Andrew.
Wanashindwa
kuwa na maelewano mazuri ndiyo maana wamekuwa wakiruhusu goli katika michezo
mingi hivi sasa-hata dhidi ya Kiluvya, Ngaya ambazo ni timu dhaifu. Andrew bado
kijana na anachipukia vizuri lakini uzoefu alioupata Mtibwa Sugar bado
haujadhihirisha ubora wake katika kikosi cha Yanga, wazoefu Kelvin, Nadir na
Bossou wote wamekuwa wakijichanganya na kuruhusu Dida kuwa matatizoni mara kwa
mara.
Kuanzia
katika beki za pembeni,Kessy/Abdul katika beki namba mbili,Mwinyi Hajji na
Oscar Joshua katika beki namba tatu hadi kwa walinzi wa kati Yanga wanapaswa kuongeza uwezo wao wa kiutulivu, kimbinu na
kiakili. Hii ni nafasi yao ya wazi kufuzu kwa hatua ya makundi.
No comments:
Post a Comment