TANGAZA NASI HAPA

Tuesday, 7 March 2017

Jicho la 3: Tatizo la Msuva ni kuichezea klabu kubwa, si kukosa penalti...




 Na Baraka Mbolembole

TATIZO la Saimon Msuva si kukosa penalti, tatizo kwake ni kuichezea klabu kubwa zaidi nchi Tanzania.

Msuva amekuwa akikosolewa sana na mashabiki wa klabu yake. Si yeye tu, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, na sasa mashabiki wa Yanga wamehamia hadi kwa mlinzi wa kati Mtogo, Vicent Bossou na mshambulizi Mzimbabwe, Donald Ngoma.

Najiuliza mara kwa mara ni kwanini mashabiki wa Yanga wanasahau mapema msaada uliotolewa/unaoendelea kutolewa na wachezaji hao katika timu yao.?!

Chanzo cha mashabiki wa Yanga kumzomea mara kwa mara Msuva na kumkosoa Niyonzima ni kwasababu 'wanaamini' wachezaji hao 'wana mapenzi na mahasimu wao Simba SC.

Msuva ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga, ana akili sana pindi unapomweleza jambo ndio maana ninaamini baadhi ya mashabiki wa klabu yake wanakosea sana wanapomtuhumu mchezaji ambaye alifunga magoli 17 na kushinda tuzo binafsi ya mfungaji bora katika ligi kuu Tanzania bara misimu miwili iliyopita.

Wanakosea zaidi wanamtuhumu kucheza chini ya kiwango wakati tayari amehusika kikamilifu katika magoli zaidi ya 20 ya timu katika ligi inayoendelea hivi sasa. Tangu alipoingia katika timu hiyo akiwa kinda wa U19 mwaka 2012 hadi sasa akiwa na miaka 23 bila shaka kiungo huyo mshambulizi wa pembeni amefanya jitihada kubwa na ataendelea kufanya vizuri kutokana na utulivu wake.

 Kama mchezaji aliyeingia Yanga akiwa hana uzoefu, Msuva amesimamiwa na makocha, Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji, Waholland, Ernie Brandts na Hans van der Pluijm, raia wa Brazil, Marcio Maximo na sasa anaendelea kukua vizuri kimchezo chini ya Mzambia, George Lwandamina.

Naamini kama mwanadamu amelinda 'utu' wake, hana ubinafsi na amekuwa akicheza kitimu ili kupata mafanikio ndiyo maana katika misimu yake mitano klabuni hapo amefunga zaidi ya magoli 60, ameisaidia klabu kushinda mataji matatu ya ligi kuu (2012/13, 2014/15, na 2015/16)

Amekuwa mstali wa mbele kupigania taji la tatu mfululizo la klabu, amesaidia mataji mawili ya Ngao ya Jamii na moja la michuano ya FA Cup, pia alikuwa ni sehemu ya wachezaji muhimu walioisaidia Yanga kufuzu kwa mara ya kwanza katika hatua ya makuodi ya Caf Confederation Cup 2016.

Msuva amekuwa katika kiwango bora kabisa kwa misimu mitatu sasa, na anaweza kufikia mafanikio makubwa zaidi kama mashabiki wa klabu yake wataendelea kuwa upande wake japokuwa mashabiki ni 'watu wanaopenda kupita kiasi' hivyo wanataraji mambo mazuri tu kila wakati.

Mataji aliyoisaidia klabu kuyapata, rekodi zake za ufungaji na umahiri wa kujitolea kwa ajili ya timu haviwezi kufunikwa na 'ukosefu wake' wa mkwaju wa penalti katika mchezo muhimu dhidi ya
Mtibwa Sugar siku ya jana Jumapili.

Nimemsikia akisema alipaisha penalti ile kutokana na 'imani ya kishirikina' siamini kama ni kweli
kwa sababu ile tayari alikwishapoteza penalti mbili ndani ya miezi mitatu ya mwaka huu. Inawezekana hakuna mchezaji mwingine anayejiamini katika upigaji wa mikwaju ya penalti katika tinu ya Yanga kama Msuva ndiyo maana amekuwa akiendelea kubeba majukumu hayo licha ya kupoteza mara kwa mara.

Yanga kama timu imekosa kujiamini katika upigaji wa mikwaju ya penalti kwa miaka zaidi ya miwili sasa. Na kwa timu inayocheza mara kwa mara katika michuano ya 'mtoano' inaonesha wazi hawafanyi mazoezi ya kutosha katika eneo hilo.

Baada ya kupoteza mkwaju wa penalti siku ya jana wengi wa mashabiki wa Yanga wanahoji ni
kwanini Nahodha, Nadir hakukwenda kupiga au Kelvin Yondan? Upande wangu nadhani hilo ni tatizo la timu nzima ndiyo maana katika miaka ya karibuni magolikipa, Ally Mustapha na Deo Dida wamekuwa wakijibebesha majukumu hayo lakini nao tumeshuhudia wakipoteza mara kadhaa.

 Jambo la kuhoji hapa ni je, timu imekuwa ikifanya mazoezi ya kutosha katika upigaji wa penalti.? Penalti anaweza kupoteza mchezaji yeyote yule hivyo Msuva asilaumiwe kiasi cha kumpunguzia uwezo na ufanisi wake kiuchezaji kwa sababu ni mchezaji anayecheza ili kushinda mechi.

Mashabiki wabadilishe mitazamo yao mibaya na wawe na kumbukumbu na yale ambayo yamekuwa yakifanywa na wachezaji wao. Msuva 'aweke pamba masikioni' na achukulie kelele za lawama zinazoelekezwa kwake kama changamoto za kuichezea klabu kubwa, yenye mashabiki wengi na
inayofuatiliwa sana.

No comments:

Post a Comment