Na Baraka Mbolembole
MAKAMU bingwa wa ligi kuu Tanzania Bara na FA Cup, timu ya Azam FC inataraji
kumkaribisha tena kikosini nahodha na mshambuaji wao namba moja John Bocco
katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Stand United siku ya kesho Jumamosi katika
uwanja wa Azam Complex Chamanzi.
Azam FC ambayo iliifunga Mtibwa Sugar na kutinga robo fainali katika
michuano ya FA inataraji kuutumia mchezo huo dhidi ya Stand kama maandalizi ya
mwisho kuelekea mchezo wa Caf Confederatio Cup dhidi ya
Mbabane Swallows F.C mwishoni mwa wiki ijayo.
“ Tunamshukuru Mungu maandalizi yetu yanaendelea vizuri,kasoro pekee ni
kwamba tutaendelea kukosa huduma ya kiungo wetu raia wa Cameroon, Stephan Kingu
ambaye alipata majeraha katika mchezo wetu dhidi ya Simba mwezi uliopita, lakini
habari nzuri ni kwamba John Bocco amerejea na atakuwepo kwenye mchezo wa kesho
panapo majaliwa kama mwalimu ataamua kumtumia. Kiujumla maandalizi yako sawa
hadi sasa.” Anasema meneja wa Azam FC, Phillip Alando.
“ Kocha anauchukulia kwa umuhimu mkubwa mchezo huo ukizingatia kwamba tulimfikishia
taarifa za kupoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza kule Shinyanga dhidi ya hawa
Stand kwa hiyo mwalimu anaiona kama timu ambayo inapigana hivyo hana mzaha
kabisa katika maandalizi yake kuelekea
mchezo huo.”
Azam FC ilifungwa 1-0 katika uwanja wa Kambarage katika mchezo ambao mlinzi
wa timu hiyo Aggrey Morris alimchezea vibaya mshambulizi wa Stand, Chidiebele
Abasarim kiasi cha kupelekea Mnigeria huyo kuvunjika taya.
“ Kocha anahitaji pointi tatu ili kufanya timu iwe katika nafasi nzuri
zaidi kwenye ligi. Nachoweza kuwaambia mashabiki wa Azam kwamba, tutajitahidi
kuchezavizuri ili kupata ushindi na niwaombe waje kwa wingi ukizingatia kwamba
mechi yetu ya kesho itakuwa ya mwisho kabla hatujacheza mchezo wetu dhidi ya
Mbabane Swallows kwenye michuano ya Confederation, hivyo waje kutazama nini
ambacho mwalimu amekiandaa kuelekea mchezo wa Caf.”
No comments:
Post a Comment