GOLI pekee lililofungwa na mshambulizi, Vicente Iborra dakika ya 14’ lilisimama hadi
mwisho wa mchezo na kuwapa wenyeji Sevilla ushindi wa
goli 1-0 dhidi ya Athletic Bilbao
katika pambano la ligi kuu Hispania-La Liga usiku wa Alhamis hii
katika dimba la Ramon Sanchez Pizjuan.
Mkwaju wa penalty uliopigwa na kiungo-mshambulizi, Steven
Jovetic dakika ya 14’ uliokolewa kwa miguu
na golikipa wa Bilbao, Gorka Iraizoz Moreno lakini Iborra aliuwahi mpira huo
uliokolewa na kupiga kiki ya karibu iliyompita kwenye kwapa kipa huyo wa
Bilbao na kuiandikia Sevilla goli hilo
pekee.
Vijana hao wa kocha Muargentina, Jorge
Sampaoli wameendelea kuwabana vigogo FC Barcelona na Real Madrid katika mbio
za ubingwa baada ya kufikisha pointi 55 ( alama mbili nyuma ya vinara
Barcelona na pointi moja nyuma ya Real)
Katika mchezo mwingine uliopigwa Alhamis hii, Atletico
Madrid bado wameendelea kuwa na msimu mgumu katika La Liga baada ya kulazimika
kusawazisha goli la dakika ya 13’ la Florin
Andone na kuambulia sare ya kufungana 1-1 dhidi ya Deportivo La Coruna katika
dimba la Riazor.
Mshambulizi wa Ufaransa, Antoine
Griezmann alifunga goli la kusawazisha dakika ya 68’. Kufuatia sare hiyo
Atletico wamesalia nafasi ya nne katika
msimamo wakiwa na pointi 46 baada ya kucheza michezo 25 huku wakifuatwa
kwa karibu na Real Sociedad ambao wana
alama 45.
LIGI hiyo itaendelea leo Ijumaa kwa mchezo mmoja
utakaozikutanisha timu za Real
Betis na Sociedad.
No comments:
Post a Comment