TANGAZA NASI HAPA

Tuesday, 7 March 2017

Mwambusi: Bado tunaweza kushinda VPL, njooni kuisapoti timu leo vs Kiluvya...





 Na Baraka Mbolembole

LICHA ya kuangusha pointi tano katika michezo mitatu iliyopita ya ligi kuu ya kandanda Tanzania bara, mabingwa watetezi wa ligi hiyo ni michuano ya FA Cup, timu ya Yanga SC bado inaamini inaweza kushinda wa ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo msimu huu.
  
Kikosi hicho kilichokusanya pointi 53 katika michezo 24 ya VPL kinataraji kuwavaa Kiluvya United ya Pwani katika mchezo wa hatua ya 16 bora katika TFF Confederation Cup 2016/17.

" Bado tutaendelea kukosa huduma za baadhi ya wachezaji wetu katika mchezo wa Jumanne hii dhidi ya Kiluvya kutokana na majeraha waliyonayo. Hatuwezi kuanza kufikiria mchezo wa Zanaco wakati tunakabiliwa na mchezo mwingine muhimu katika michuano ya FA." anasema kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi.

" Hatutakuwa na Donald Ngoma, Haruna Niyonzima, Juma Abdul lakini wachezaji tulio nao tuwaamini, wacheza vizuri, wanajituma, wanajitolea kwasababu ya Yanga. Tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ili kufuzu kwa robo fainali. Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru watu wote wa Yanga, wamekuwa wakiandamana na sisi kila mahala licha ya kwamba kuna wakati matokeo yanakuwa 'machache' lakini tunashukuru Mwenyezi Mungu na tunawashukuru wao." anasema Mwambusi .

Yanga  ilipoteza 2-1 dhidi ya Simba kisha wakashinda 2-0 mbele ya Ruvu Shooting, Jumapili iliyopita wakalazimisha suluhu-tasa dhidi ya Mtibwa Sugar katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

 " Vijana walipambana katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa lakini tukakosa bahati kidogo na kupata matokeo tuliyopata ya pointi moja, matokeo hayo hayatoshi kusema sisi tumetoka katika mbio za ubingwa, lakini vilevile nawaomba mashabiki wetu wazidi kutuunga mkono. Waje kwa wingi katika mchezo wetu wa leo ili kuwapa motisha vijana, kuwahamasisha ili tuweze kufanya vizuri zaidi katika mchezo ambao ni 'wa mtoano,' ukishinda unaendelea, ukishindwa una nje ya michuano."

No comments:

Post a Comment