MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya
kandanda Tanzania bara, timu ya Yanga SC leo itakuwa na kibarua kigumu ugenini
Jamhuri Stadium, Morogoro itakapowakabili Mtibwa Sugar FC katika muendelezo wa
michezo ya ligi kuu ya Vodacom.
Yanga inashika nafasi nyuma ya vinara
Simba SC na ushindi wa aina yoyote katika mchezo wa leo utawapeleka kileleni
kutokana na wastani wao mzuri wa magoli ya kufunga na kufungwa.
Baada ya kulazimishwa sare ya
kufungana 2-2 na Mbeya City FC siku ya jana Jumamosi, Simba wanaongoza ligi
wakiwa na alama 55(pointi 3 mbele ya Yanga wanaoshika nafasi ya pili.)
Ushindi katika uwanja wa Jamhuri leo
kwa kikosi cha kocha Mzambia, George Lwandamina utawafanya mabingwa hao
watetezi kurejea kileleni kutokana na wastani wao mzuri wa magoli.
Katika michezo 24 waliyokwishacheza Simba
imefanikiwa kufunga magoli 40 na kuruhusu nyavu zao mara kumi hivyo kuwa na
wastani wa magoli 30, wakati Yanga katika michezo 23 waliyokwishacheza
wamefanikiwa kufunga magoli 49 na kuruhusu magoli 11 hivyo kuwa na wastani wa magoli
38.
Yanga imefanikiwa kushinda mara moja
tu katika uwanja wa Jamhuri tangu mwaka 2009 dhidi ya Mtibwa huku ushindi wao
pekee ukiwa ule wa 2-0 katika mchezo wa raundi ya kwanza msimu uliopita.
Mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa
ambaye alioneshwa kadi nyekundu ya utata katika mchezo wa Jumatano iliyopita vs
Ruvu Shooting amefutiwa adhabu hiyo na Kamati ya masaa 72 hivyo atawavaa Mtibwa
katika mchezo wa leo.
' Wakata miwa' hao wa Turiani, Morogoro wapo
nafasi ya tano katika msimamo wakiwa na pointi 33 baada ya kucheza michezo 23.
Mchezo mwingine leo Jumapili
utapigwa katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam utazikutanisha African Lyon
iliyo nafasi ya 14 na pointi 23 dhidi ya Mwadui FC iliyo nafasi ya 6 na alama
31.
No comments:
Post a Comment