TANGAZA NASI HAPA

Tuesday, 28 February 2017

VPL: Yanga SC kuivaa Ruvu Shooting Leo bila Donald Ngoma




 Na  Baraka Mbolembole

BAADA  ya  kupokea  kipigo  cha  2-1  kutoka kwa mahasimu  wao  Simba  SC  siku  ya  Jumamosi  iliyopita,mabingwa  watetezi  wa  ligi  kuu  Tanzania  Bara, timu  ya  Yanga  SC  Leo Jumatano  itashuka  uwanja  wa  Taifa  Dar  es  Salaam kuwavaa  Maafande  wa  Ruvu  Shooting katika  muendelezo wa  michezo  ya  ligi  kuu.

 Yanga  ilikuwa  ikijifua  tangu  Jumatatu  lakini  kwa  mara nyingine  wataingiza  timu  yao  uwanjani  bila  huduma  ya  mshambulizi  Mzimbabwe, Donald  Ngoma  ambaye  bado  anasumbuliwa  na matatizo ya  goti.

Ikiwa  na  pointi 49  baada  ya  kucheza  michezo 22 kikosi  hicho  cha  kocha  Mzambia, George  Lwandamina  kitalazimika  kushinda ili  kupunguza  ‘gepu’  la  pointi  tano dhidi  ya  vinara  Simba  ambao  tayari  wamecheza  michezo 23.

Yanga  imeingia  katika  kipindi  kingine  kigumu  msimu  huu  baada ya kupoteza  mchezo  wa  tatu  Jumamosi  iliyopita. Mara  baada  ya  kucheza  na  Shooting  timu  hiyo itasafiri  hadi  mkoani Morogoro  kuwavaa  Mtyibwa  Sugar  katika  uwanja  wa  Jamhuri sehemu  ambayo  wamefanikiwa  kushinda  mara  moja  tu  katika  miaka  nane  iliyopita.

 “  Timu imejiandaa vizuri, naweza kusema  maandalizi  kuelekea  mchezo  wa  Jumatano  hii yameshakamilika. Timu  ilikuwa  ikifanya  mazoezi  tangu  siku  ya  Jumatatu, jana  pia walifanya  mazoezi  ya  jioni sasa  wako  kambini tunasubiri  jioni  waingie  uwanjani kucheza  mechi.”  Anasema  Mkwassa mchezaji  na  kocha  wa  zamani  wa  klabu  hiyo.

“ Sisi  kama  uongozi  tunajua  tunakwenda  kucheza  mechi  nyingine ngumu, vijana  itabidi  wajipange  vizuri ili  kuweza  kupata  matokeo mazuri. Kama  unavyojua  mechi  iliyopita  hatukupata  matokeo  mazuri kwa  hiyo  ili  kuwaamsha  tena  mashabiki  wetu tunahitaji  kupata  matokeo mazuri ili  kurudisha  moto  tuliokuwa nao. Jukumu  kubwa  ni  la  wachezaji pamoja  na  benchi  la  ufundi kuweza  kuamsha  hiyo  morali  na  sisi  kama  uongozi  tuko  nyuma  yao.”

 “ Kuhusu  Donald  Ngoma  ni  kwamba  taarifa  nilizokuwa nazo  ni  kwamba bado  anasumbuliwa  na  majeraha hivyo  hatoweza  kutumika  katika  mchezo  wa  Leo.”

No comments:

Post a Comment