TANGAZA NASI HAPA

Monday, 27 February 2017

Jicho la 3; ‘ Si Kamusoko, Lwandamina, Ndemla ndio waliipoteza Yanga …’



Na Baraka  Mbolembole


KOSA la kwanza la kocha, George Lwandamina ni kumuacha benchi nahodha, Nadir Haroub na kumuanzisha Vicent Andrew katika nafasi ya beki wa kati. 
 
Kocha wa Simba, Joseph Omog hasingeweza kuepuka kumpanga Novatus Lufunga kama mlinzi-pacha wa Abdi Banda kutokana na majeraha ya Mzimbabwe, Method Mwajale. 

Kabla ya mechi niliandika katika 'Jicho la 3' kwamba, Simba hawapaswi kuwaanzisha washambuliaji wake watatu, Laudit Mavugo, Juma Liuzio na Ibrahim Ajib. Pia nilisema ili 'kujaribu' kuifunga Yanga, Omog anapaswa kuwapanga James Kotei, Said Ndemla, Muzamiru Yassin na Mohamed Ibrahim.


PENALTI DAKIKA YA 3' 

Mzambia, Obrey Chirwa alilazimisha kumpita mlinzi wa kati wa Simba, Lufunga. Akitambua fika yupo ndani ya eneo la hatari huku Lufunga akiwa nyuma yake, Chirwa alikimbia 'kikakamavu' lakini 'alilegea' na kuanguka baada ya mguu wa kushoto wa Lufunga kumgonga kwa nyuma katika mguu wake wa kushoto. Ilikuwa penalti dhahiri iliyoambatana na kadi ya njano kwa mlinzi huyo wa Simba.


 MABADILIKO YA KWANZA-KUMTOA LIUZIO NA KUMPA NAFASI NDEMLA DAKIKA YA 26' 


Kitendo cha kuwapanga kwa wakati mmoja Mavugo, Liuzio na Ajib ndiyo kulifungua nafasi ya Justine Zulu, Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima na Msuva kutawala kiungo cha Simba. Nilisema awali kuwa
washambuliaji hao watatu wa Simba huwa hawana msaada mkubwa kiukabaji.

Zulu alikuwa akikaba na 'kuua' njia zote za viungo wa Simba kupeleka pasi kwa washambuliaji wao. Kamusoko aliichezesha timu kwa kasi huku pia akiwa makini katika ukabaji, ili kuwarudisha mchezoni wachezaji wake ambao waliopotezwa na mkwaju wa mapema wa penalti, kocha Omog alichukua uamuzi sahihi ambao alipaswa kuufanya kabla ya kuanza kwa mchezo. 

Kitendo cha kocha huyo kumtoa Liuzio na kumpa nafasi Ndemla dakika ya 26' kilimpa faida kama kocha kwa kufanya mabadiliko yaliyokuwa na faida. Ndemla ni kiungo mwenye uwezo wa kupiga pasi za
umbali mrefu na kuwafikia walengwa.

Baada ya kuingia kwa Ndemla, Simba ikabadilika kiuchezaji. Walipata nyongeza ya pasi ndefu zilizofika. Kotei, Muzamiru na Mohamed Ibrahim wote si wazuri katika pasi ndefu ndiyo maana walisumbuliwa sana na viungo wa Yanga kwa sababu ya uchezaji wao wa pasi fupifupi.

KUUMIA KWA THABAN KAMUSOKO DAKIKA YA 45' 
 Awali raia huyo wa Zimbabwe alionekana kuwa na siku njema. Lakini mambo yakaja kubadilika mara
baada ya kuingia uwanjani Ndemla ambaye aliituliza safu ya kiungo ya Yanga kutokana na mchezo wake wa kupiga pasi ndefu ambazo ziliwafanya hata wachezaji wa Yanga kuanza 'kukimbizwa.' 

Kamusoko alijikuta akitumia nguvu nyingi zaidi na jambo hilo likapelekea kujitonesha maumivu yake ya goti.
Japokuwa alijikaza na kuendelea kucheza kwa dakika tano lakini kadri Simba walivyoongeza kasi katika uchezaji wao, Thaban akalazimika pia kuongeza spidi na matumizi ya nguvu jambo ambalo lilimuongezea maumivu zaidi. Dakika 15 za mwisho kuelekea muda wa mapumziko Simba walitawala mchezo.

KAMARI ILIYOZAA HASARA NA FAIDA KWA SIMBA 
 Dakika 6 baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, kocha wa Simba, Omog aliamua 'kucheza kamari.'
Alimpumzisha mlinzi wa kati, Lufunga na kumpa nafasi kiungo mshambuliaji wa pembeni, Shiza Kichuya. Nadhani Omog alifanya hivyo ili kuilinda timu yake isicheze pungufu kwa kuhofu huenda Lufunga
angepata kadi nyekundu. 

Mlinzi wa kulia, Mcongoman Besala Bokungu akaenda kucheza beki ya kati sambamba na Banda, Muzamiru akarudishwa chini zaidi katika beki namba mbili na kwa vile katikati ya uwanja walikuwepo Mohamed Ibrahim, Ndemla na Kotei, kocha huyo hakuona hatari yoyote kumpa nafasi Kichuya kwa sababu upande wa kushoto wa Yanga haukuwa na madhara.

Dakika nne baada ya Bokungu kuhamia nafasi ya beki wa kati akalambwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea vibaya Chirwa ambaye alishamuacha mlinzi huyo wa Simba na bila kuchezewa faulo bila shaka angeenda kufunga. Kile ambacho Omog alikihofia kumtokea Lufunga kikamtokea Bokungu na kuwaacha wakibaki pungufu huku wakiwa nyuma 1-0.

ALICHOPASWA KUFANYA LWANDAMINA BAADA YA SUB YA LUFUNGA 
 Simba walimtoa beki na kumuingiza kiungo mshambuliaji, lengo lao lilikuwa ni kuongeza nguvu katika mashambulizi. Kama kocha huku pia timu yake ikiwa mbele, Omog alipaswa kumpa nafasi Geofrey Mwashuiya ambaye ni wing mzuri mwenye mbinu, kasi na uwezo wa kumiliki mpira. 

Kwa kutambua kuwa Muzamiru ni mchezaji wa kiungo, Mwashuiya angeweza kumsumbua sana na
pengine kumfanya hadi Kichuya arudi nyuma kumsaidia beki wake namba mbili. 

Lakini wala kocha huyo raia wa Zambia hakuwa na habari. Kuondolewa uwanjani kwa Bokungu huku Simba wakiwa hawana mchezaji mwingine wa nafasi ya beki, Lwandamina alipaswa kumpa nafasi Emmanuel Martin na mambo yangekuwa vizuri upande wao.

Baada  ya  kushindwa  kupanga  timu  yake vizuri,  Lwandamina  alishindwa  pia  hata  katika ufanyaji  wa  mabadiliko  na  yale  aliyoyafanya  hayakukidhi  ubora wa  mechi na  alifanya  katika  muda  mbaya.

KOTEI, NDEMLA, KICHUYA ‘NAWAPA  TANO’


Mara  baada  ya  kuondolewa  uwanjani  kwa  Bokungu, Mghana,Kotei  alienda  kucheza  katika  beki  yakati  sambamba  na  Banda. Uchezaji  wake  ulikuwa  zaidi   ya  beki,  alizuia  na  kuipeleka  timu  mbele kwa  kasi  kasha  alirudi  haraka  katika  eneo  lake  la  ulinzi. Na  alipogundua  nguvu  ndogo  ya  Yanga katika mashambulizi  akaamua  kucheza  kama  namba  6. Huyu  ni  mchezaji  wa ukweli. 



Ndemla  aliendelea  kuthibisha  kuhusu  ninachokisema  mara  kwa  mara  kuwa huyu  ndiye  kiungo  bora zaidi  Mtanzania  kwa  wale  wachezesha  timu. Alipiga  pasi  zilizofika,  alikaba  na  kuichezesha  timu.
Nilipenda  pia  moyo  wa  kipiganaji  wa Kichuya  ambaye  aliamua  kuutafuta  mpira  kila  mahali,  kusaidia  kukaba . pasi  yake  ilizaa  goli  la  kusawazisha  na baadae  akafunga  goli  la  ushindi  zikiwa  zimesalia  dakika 9  mchezo kumalizika. 

Kutoka  nyuma  1-0  huku  wakiwa  pungufu  kuanzia  dakika  ya 55’ na  kushinda  2-1  dhidi  ya  Yanga, sawa  kuna  vikosi  vya  Simba  vilishafanya hivyo  dhidi  ya  Yanga  lakini  ushindi  huu  wa  juzi,  niliona  jitihada  kubwa  za  wachezaji ,  benchi  la  ufundi, Simba  walitumia  ‘udhaifu’  na  uwezo  mdogo  wa  kocha  Lwandamina  katika  usomaji  wa  mchezaji  na  wakashinda  kwa  haki.

No comments:

Post a Comment